Breaking

Fahamu Taratibu za kupata kitambulisho upya kutoka NIDA


Kwa muda mrefu kumekuwepo hitaji la wananchi kujua utaratibu wa kupata kitambulisho kipya baada ya kile cha awali kupotea.

Related image

Zipo sababu nyingi zinazoweza kusababisha mtu kuhitaji kupata kitambulisho kipya kama:-

- Kitambulisho kupotea/kuteketea kutokana na majanga kama vile moto, mafuriko

- Wizi

- Kitambulisho kuharibika

- Kubadilisha majina kwa sababu mbalimbali

- Au majina kukosewa.


Kwa kutambua uwepo wa mahitaji haya msingi, NIDA tumeona ni vema kuweka bayana katika jamvi hili taratibu zote za msingi zitakazokuwezesha kupata kitambulisho kingine kwa wakati.


Hatua hizi ni muhimu kufuatwa ili kukuwezesha kupata kitambulisho kingine kwa wakati.


Muhimu kuzingatia yafuatayo; unapopata Kitambulisho cha Taifa kwa mara ya kwanza, nakili namba yako ya utambulisho mahali salama. Hii itakusaidia iwapo utakipoteza kwa kuibiwa au kupata janga lolote, kwa kutumia namba ya usajili utaweza kuendelea kupata huduma mbalimbali kama kawaida wakati ukisubiri kupatiwa kitambulisho kipya. Hili linawezekana kwa kuwa utambulisho wako upo kwenye mfumo wa kielektroniki.


1. Kubadilisha Taarifa


Kwa mwenye kitambulisho ambaye ambaye anataka kubadili taarifa zake na hivyo kuhitaji kitambulisho kuchapishwa upya atafanya yafuatayo:-


1.Mwombaji atapaswa kuandika barua NIDA kueleza sababu za msingi za kubadilisha taarifa zake katika mfumo na kuambatanisha hati msingi za kisheria zenye kuruhusu kufanya hivyo. Mfano iwapo atataka kubadili majina lazima kufika na hati ya kisheria ijulikanayo kama “deed poll”.

2.Mwombaji atajaza fomu ya maombi katika ofisi ya NIDA kwenye Wilaya anayoishi

3. Atatakiwa kulipia benki ada ya shs. 20,000/- kama gharama za kuchapisha upya kitambulisho chake.

4. Akisha kufanya malipo, atawasilisha stakabadhi ya malipo ya benki na kupata stakabadhi ya serikali kutoka ofisi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

5. Baada ya kukamilika utaratibu huo, atapewa muda wa kusubiri kabla ya kufika kwenye ofisi ya NIDA kupewa kitambulisho kingine.



2. Kupoteza kitambulisho kwa kuibiwa au kwa majanga


Mwombaji aliyepoteza kitambulisho chake kwa kuibiwa au kwa majanga,atapaswa kufika katika ofisi ya NIDA kwenye Wilaya anayoishi na kuthibitisha taarifa zake kabla ya kupewa barua ya utambulisho kwa Polisi, barua ambayo itakuwa na namba yake ya utambulisho. Kupitia barua hiyo Polisi watampatia uthibitisho wa upotevu wa kitambulisho chake “Police Loss Report”. Kisha mtuamiaji atapaswa kufanya yafuatayo ili kupata kitambulisho kipya


1. Mtumiaji atawasilisha ripoti ya upotevu kutoka Polisi; katika ofisi ya NIDA Wilaya anayoishi na kujaza fomu maalumu.

2. Atatakiwa kulipia benki ada ya shs. 20,000/- kama gharama za kuchapisha upya kitambulisho chake.

3. Akisha kufanya malipo, atawasilisha stakabadhi ya malipo ya benki na kupata stakabadhi ya serikali kutoka ofisi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

4. Baada ya kukamilika utaratibu huo, atapewa muda wa kusubiri kabla ya kufika kwenye ofisi ya NIDA kupewa kitambulisho kingine.


Muhimu kufahamu; Vitambulisho vya Taifa kwa mara ya kwanza hutolewa bure kwa raia, na pindi kinapochapishwa upya raia hana budi kulipia kufidia gharama za uchapaji. Hivyo tunasisitiza ni muhimu wananchi kutunza vitambulisho vyao kuepuka gharama.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.