Shirika Lisilomuamini Mungu Kuwazawadia Watahiniwa Waliofeli Masomo ya Dini
Shirika la watu wasioamini uwepo wa Mungu nchini Kenya (AIK) limetangaza kuwazawadia watahiniwa waliofeli zaidi kwenye masomo ya dini katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2017.
Shirika hilo limewataka wanafunzi wote waliopata alama E kwenye mtihani huo kutuma maombi, likitangaza kuwa wanafunzi wawili bora wa kiume na wa kike watapokea Sh10,000 ya Kenya kila mmoja.
Katika tangazo linalozunguka mitandaoni, shirika hilo limesema kuwa nia ya tuzo hizo ni kuendeleza pingamizi dhidi ya Imani za kidini na kusherehekea matokeo mabaya katika masomo ya dini.
“Tunatoa zawadi ya Sh10,000 kwa wanafunzi waliopata alama ya E katika masomo ya dini ya CRE, IRE na HRE katika matokeo ya mtihani wa 2017. Hatutaki mhisi kuwa mlifeli katika masomo haya. Kinyume chake mlifanya vyema sana,” umesema ujumbe huo.
Shirika hilo linasema litazawadia mvulana na msichana bora zaidi (kwa maana ya waliofeli zaidi) baada ya maombi kutumwa na kupitiwa kwa kina.
“Tutapitia maombi yatakayotumwa ili kubaini washindi. Ili kushiriki, lazima mmoja awe alipata alama ya E katika mtihani wa KCSE katika moja ya masomo ya dini, na watakaoshinda watachapishwa katika mtandao wetu mnamo Januari 10 na kualikwa kupewa zawadi zao katika sherehe itakayoandaliwa", imesema taarifa hiyo.
Tangazo hilo aidha linasema kuwa si lazima kwa mmoja kuwa muumini wa imani zao ili kushiriki, ila tu yeyote aliyefanya mtihani mwaka huu na akapata alama E.
Hakuna maoni: